Loading...

BREAKING NEWS: KAMANDA HUYU AJIAPIZA KUDHIBITI UKUTA

Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Dodoma
KAULI za vitisho bado zinaendelea ambapo sasa viongozi wakuu wa jeshi hilo, wanaeleza dhamira ya kutumia nyembo mbalimbali kuhakikisha operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) inazimwa, anaandika Dany Tibason.
Operesheni hiyo ilitangazwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Julai mwaka huu baada ya kufanyika Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi amesema, atatumia kila nyenzo kuzima Ukuta.
Kauli hiyo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari mjini hapa, ikiwa ni siku moja tangu Mbowe, atangaze msimamo wao kwamba, maandamano hayo yatafanyika kama ilivyopangwa.
Amesema, jeshi hilo lina majina ya wanachama wa Chadema wanaopita nyumba kwa
nyumba kuhamasisha watu washiriki maandamano hayo.
Na kwamba, wengine wamejipanga kushambulia polisi hivyo amewataka kutambua kuwa, jeshi hilo lina uchungu wa kuondokewa na askari wenzao walioshambuliwa na baadhi kupoteza maisha hivyo hawako tayari kuendelea kuchezewa.
Hata hivyo, alipotakiwa kutaja majina ya watu hao Mambosasa amesema, yatatajwa baada ya kuwakamata kwasababu, angeyataja wangeweza kutorokea mikoa mingine.
“Serikali siyo polisi pekee, vyombo vya usalama ni pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kata, viongozi wote wa serikali za mitaa, wakaguzi wa
tarafa na polisi kata ambao wanategemewa kukusanya na kutoa taarifa za
kiintelijensia, tutatumia nyenzo zote kuhakikishia wananchi usalama
wao na mali zao,” ameseleza Mambosasa.
Wakati Mambosasa akisema hivyo, Jerad Mambo, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Dodoma amesema, mikakati yao imekamilika na vijana wana ari ya kutetea haki yao.
Geofrey Mwakiseyo, Katibu wa Chadema wa Jimbo la Mpwapwa amesema, mpaka sasa watu wa kada tofauti katika vitongoji 39 wapo tayari kwa maandamano hayo.
Kuhusu zuio lililotolewa na Kamishna Mambosasa, Mwakiseyo amesema,
anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi kama ambavyo na wao watatekeleza majukumu yao ya kisheria na Katiba hiyo hiyo, kupitia Ukuta.
Kamishna Mambosasa amewataka wanahabari kutohofia usalama wao na kufanya kazi zao hususan kuhusu hali itakavyokuwa siku hiyo ya Septemba Mosi.

BREAKING NES: Taarifa Muhimu Kwa Umma Kutoka JKT



  TAARIFA KWA UMMA

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linapenda kukanusha taarifa potofu zinazosambazwa kwa njia ya ujumbe mfupi kwenye baadhi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii inayoeleza kuwa” JKT linawataka vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa Kujitolea mwaka 2016, waripoti ofisi za wakuu wa mikoa kati ya terehe 03 – 07 Septemba 2016, tayari kwa kupelekwa kwenye Makambi ya mafunzo ya JKT”.

Taarifa hiyo siyo sahihi na wananchi wanatakiwa kuzipuuza. Utaratibu utakapokamilika wa kuwachukua Vijana hao, JKT itawatangazia kupitia vyombo rasmi vya habari na siyo kwa njia ya simu za mkononi.

Aidha JKT kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini inafuatilia kujua ni mtu gani au kikundi gani kimehusika na upotoshaji huo wa taarifa ili hatua kali za kisheria kuchukuliwa.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya JKT
27 Agosti 2016

BREAKING NEWS: VIKINDU PAMOTO KIKOSI MAALUMU CHA JESHI LA POLISI KUFANYA KAZI YAO UMATI WASHUDIA TUKIO HILI

HALI ya taharuki imetanda baada ya usiku mzima wa kuamkia jana Kikosi Maalumu cha Jeshi la Polisi cha Kupambana na Uhalifu, kupambana na genge la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi katika nyumba waliyokuwa wakiishi eneo la Vikindu, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani. 

Katika mapambano hayo ambayo msingi wake ni operesheni ya kuwasaka watu walioua askari wanne wiki hii, inadaiwa Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Uhalifu, Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Thomas Mniko, aliuawa. 

Mniko anadaiwa kupigwa risasi na watu hao wanaodaiwa kuwa na utaalamu wa kutumia silaha nzito chini ya kiongozi wao anayedaiwa kuwa ni Luteni Kanali mstaafu wa Jeshi la Wananchi aliyepata mafunzo ya udunguaji nchini Cuba. 

Wakati taarifa nyingine zikieleza kuwa Kamanda Mniko aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani, nyingine zilikuwa zikieleza kichwani.
Mbali na kifo cha Mniko, kumekuwepo na taarifa tofauti ambazo hazijathibitishwa juu ya idadi ya watu waliouawa katika tukio hilo. 

Wakati taarifa toka ndani ya Jeshi la Polisi zikidai kuwa waliouawa ni 14 huku tisa kati yao wanawake watatu wakishikiliwa na jeshi hilo, taarifa toka kwa viongozi wa eneo la Vikindu zilieleza waliouawa ni wawili.
Kutokana na uzito wa tukio lenyewe, Jeshi la Polisi liliamua kutotoa taarifa yoyote jana na kuahidi kufanya hivyo leo. 

MTANZANIA JUMAMOSI LATUA VIKINDU 

Gazeti hili lilifika eneo la tukio jana asubuhi na kushuhudia hali ya taharuki ikiwa imetanda huku askari wengi wakiwa wamezingira nyumba hiyo na zaidi wakizuia wananchi na waandishi wa habari umbali wa mita kama 100 kutoisogelea. 

Wakizungumza katika eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema walianza kusikia majibishano ya risasi toka katika nyumba hiyo iliyokuwa na wapangaji tangu saa 8 usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao milio ya risasi ilikoma jana asubuhi saa 2:30. 

Idadi ya watu waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo bado haijajulikana na kumekuwa na taarifa tofauti ambapo wapo wanaodai walikuwa wakiishi watu saba ambao ni baba, mke na watoto huku wengine wakidai ni familia mbili tofauti ambazo zilikuwa hazifahamiki.



KAULI YA OFISA MTENDAJI 

Akizungumza na gazeti hili Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Vikindu, Abass Ndambe, alisema alianza kusikia majibizano ya risasi tangu saa 8 usiku ambapo aliamua kuwaamsha majirani zake ili kujua tatizo.
“Operesheni imeanza saa 8 usiku, tulisikia mlipuko lakini hatukujua dhahiri kama ni bomu au risasi za kawaida hapo tukaamshana, lakini hatukuweza kufika eneo hilo hivyo tulisubiri hadi asubuhi ambapo tulitaka kufika ili kujua kulikoni lakini askari walituzuia,” alisema Ndambe. 

Ndambe aliyasema hayo baada ya kuitwa na kupewa taarifa juu ya tukio hilo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniveture Mushongi.
Ndambe alisema RPC huyo alimweleza kuwa walikuja kumkamata mtuhumiwa wa mauaji ya polisi wanne yaliyotokea wiki hii eneo la Mbande, Temeke jijini Dar es Salaam baada ya wenzake waliokamatwa kumtaja. 

“Katika majibizano ya risasi, RPC alisema watu wawili ambao ni askari mmoja na mtuhumiwa mmoja waliuawa. Hata hivyo, sijapata idadi ya waliokamatwa. Sijawahi kuona uhalifu mkubwa vile Vikindu ingawa kulikuwa na matukio ya uvunjaji wa maduka lakini si kwa majibizano ya risasi kama hivyo,” alisema Ndambe. 

Akisimulia kilichotokea Mwenyekiti wa Mtaa huo wa Vikindu Mashariki, Mohammed Maundu, alisema usiku wa tukio saa 8, walifika askari ambao hakuweza kujua idadi yao wakiongozwa na Kamanda Thomas.
“Askari walifika na kugonga mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi watuhumiwa ambapo hapo hapo askari mmoja akapigwa risasi ya kifuani na kufa palepale. Baada ya kifo cha askari huyo kulitokea taharuki kwa askari ndipo yakaanza majibizano ya risasi hadi saa mbili asubuhi ambapo wamefanikiwa kuwakamata watu saba wa familia moja wakiwemo watoto waliokuwa ndani ya nyumba hiyo,” alisema Maundu. 

Maundu alisema taarifa alizozipata zilidai kuwa hakukuwa na silaha iliyokamatwa jambo linaloonyesha kuwa aliyefyatua risasi iliyomuua askari huenda alikimbia.
“Waliokamatwa wamechukuliwa na askari kwa ajili ya kutoa maelezo zaidi, hivyo katika tukio zima hakuna mtuhumiwa aliyefariki,” alidai Maundu.
Alisema nyumba hiyo walikuwa wakiishi familia moja ambayo walikuwa ni wapangaji huku nje kukiwa na fremu za maduka. 

“Mimi mwenyewe sikuwahi kujua kama katika nyumba hiyo kulikuwa na watu wanaishi tofauti na wafanyabiashara wenye fremu hapa nje. 

Hakuna aliyewajua watu hawa kwa kuwa walikuwa wanaishi ndani bila kutoka nje na hata baba wa familia inaonekana alikuwa akitoka alfajiri na kurudi usiku mkubwa,” alisema Maundu. 



VYANZO VYA POLISI 

Wakati kukiwa na taarifa hizo, vyanzo vyetu vya habari toka ndani ya Jeshi la Polisi vilidai kuwa msingi wa tukio la jana ni operesheni iliyoanzishwa na jeshi hilo kwa ajili ya kuwasaka watu waliohusika na tukio la kuuawa polisi wanne wiki hii. 

“Tulianza jana (juzi) saa mbili usiku kufanya operesheni hii ambapo tulifanikiwa kuwakamata wengine, katika mahojiano walituelekeza kuwa mkufunzi wao yuko Vikindu ndipo tukaelekea huko na katika mapambano watu wawili ambao ni askari na raia walifariki dunia huku wengine wengi wakitiwa nguvuni,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilidai mtuhumiwa aliyeuawa alikuwa amejificha kwenye dari ya nyumba hivyo baada ya kumtaka kuteremka na kushindwa kutii amri walimtungua huko huko kwa kumpiga risasi. 

Akisimulia namna Kamanda Thomas alivyouawa chanzo hicho kilidai; askari walipofika eneo la tukio waliamuru watu hao kufungua mlango na kujisalimisha lakini walipogundua uwepo wa askari, watuhumiwa hao walifyatua risasi na ndipo majibizano yalipoanza na risasi ya kichwa kumpata Kamanda Thomas ambaye alifariki dunia papo hapo. 

Chanzo kingine kutoka ndani ya Jeshi hilo kilidai kuwa baada ya tukio la kuuawa askari huyo, wenzake walivunja mlango na kuanza kumimina risasi ambapo walifanikiwa kuwaua watu 14 na kuwakamata wengine watano wakiwemo wanawake wawili. 

Taarifa hizo zinashabihiana na zilizotolewa na chanzo kingine kutoka jeshi hilo ambacho kilidai kuwa katika eneo la mapambano waliuawa watu 14, askari mmoja na wengine tisa walikamatwa. 

MAZINGIRA YA NYUMBA 

Gazeti hili liliweza kuifikia nyumba hiyo ambayo mbele ina fremu tatu za maduka na kuona ikiwa imetobolewa kwa risasi ukutani, madirishani na mlango ambao ulivunjwa.
Katika nyumba hiyo yenye uzio wa tofali zilionekana nguo zenye damu na nyingine zisizo na damu zikiwa zimesambazwa chini, vyombo hasa ndoo za maji zikiwa haziko katika mpangilio mzuri hali iliyoonyesha namna mapambano yalivyokuwa makali. 

MAJIRANI 

Majirani wa nyumba hiyo (majina tunayahifadhi) waliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa walishangaa kuona kuna familia inayoishi nyumba hiyo kwa kuwa ilikuwa kimya muda wote.
“Mimi nimeshangaa kuona kuna watu wanaishi pale mie siwajui, nadhani walizuiwa kutoka ndani wakawa wanashinda uani kwao,” alisema.
Jirani mwingine, Hussein Mbando, alisema risasi zilipoanza usiku huo wa manane iliwalazimu kukesha hadi asubuhi. 

“Hatujawahi kujua kama kuna watu hatari katika eneo hili kwa kuwa hawa watu walikuwa wakiingia usiku na kutoka usiku huku wake zao wakiwa hawatoki nje hivyo hatuwajui kabisa,” alisema Mbando. 

MAKAMANDA WATUPIANA MPIRA 

Tofauti na matukio mengine ambapo Jeshi la Polisi hutoa taarifa zake mapema, jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambaye naye alikuwa katika eneo la tukio alikataa kuzungumza chochote na kuahidi kutoa taarifa kamili leo.
Awali gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, RPC Mushongi, aligoma kuzungumza na kudai kuwa mtu anayepaswa kuzungumzia suala hilo ni Kamanda Sirro kutokana na askari waliohusika kutoka kikosi maalumu. 

“Naomba muwasiliane na Kamishna Sirro ndiye anayeweza kutoa taarifa kwa sasa, ufafanuzi na maelezo zaidi,” alisema Kamanda Mushongi.
Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema atafutwe Kamanda wa Polisi Temeke au Kamishna Sirro.
Gazeti hili pia lilimtafuta kwa njia ya simu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu ambaye alisema yupo kwenye kikao. 



HALI ENEO LA TUKIO 

Katika eneo la tukio ambalo gazeti hili lilipiga kambi tangu asubuhi lilishuhudia magari ya polisi zaidi ya 10 pamoja na mengine ambayo yalikuwa na namba binafsi. 

Magari hayo yalikuwa ni pamoja na gari yenye namba PT 1860, PT 3612, gari ya RPC wa Pwani, magari mawili ya Jeshi la Zimamoto, gari ya maji ya kuwasha, gari la zimamoto na mengine.
Ilipofika saa sita kasoro mchana gari lingine la polisi lenye namba PT 3789 lilifika eneo la tukio likiwa limebeba askari wengine waliokuwa na silaha. 

Si hao tu gazeti hili pia lilishuhudia pia askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) wakiwa eneo la tukio ambalo lilikuwa limezongwa na wananchi kutoka katika viunga mbalimbali vya Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi walidai kutoka Tegeta jijini Dar es Salaam ili kushuhudia kwa kuwa walichoka kuona taarifa kwenye magazeti na runinga. 

Pamoja na hali ya usalama kuimarishwa katika eneo hilo la tukio, lakini ilipofika saa saba kasoro baadhi ya gari za polisi zilianza kupungua.
Gari moja lilibaki ili kuwasubiri Zimamoto ambao waliondoka baada ya dakika chache na kuwatangazia wananchi kuondoka eneo la tukio ili wakaendelee na shughuli zao za kila siku. 

VIZUIZI NJIANI 

Hali ya usalama barabarani ilikuwa imeimarishwa huku askari wa usalama wakiwa wametanda maeneo mbalimbali ya mkoa wa Pwani hadi Dar es Salaam.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida licha ya kuzoeleka kuwepo kizuizi kimoja tu cha polisi eneo hilo ambacho kiko Vikindu, gazeti hili lilishuhudia kizuizi kipya eneo la Kongowe ambalo ni mpaka kati ya Dar es Salaam na Pwani.
Katika kizuizi hicho, askari walikuwa na kazi ya kukakuga kila gari lililokuwa likipita eneo hilo hali iliyosababisha foleni kuwa kubwa. 

MATUKIO YA MAUAJI YA POLISI 

Ndani ya kipindi cha miaka miwili sasa kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kihalifu dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi nchini, ambapo baadhi ya askari wameuawa na wengine kujeruhiwa na watu wanaosadikiwa kupata mafunzo maalumu ya kutumia silaha.
Uvamizi huo pia umekuwa ukiambatana na uporaji wa silaha aidha kwenye vituo vya polisi, kwenye malindo au katika doria. 

Mfano wa matukio hayo ni hili lililotokea wiki hii la askari wanne kuuawa.
Majambazi hao baada ya kutekeleza mauaji hayo, walivamia Kituo cha Polisi cha Mbande kisha wakavunja stoo na kuchukua sare ya askari na silaha. 

Katika mfululizo wa mashambulizi kama hayo, Septemba 7 mwaka 2014 huko wilayani Bukombe, polisi wawili waliuawa na bunduki 10 aina ya SMG kuporwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Katika tukio hilo mbali na kupora SMG 10, pia walipora risasi ambazo idadi yake haikufahamika pamoja na mabomu ya kurusha kwa mkono. 

Juni 12, 2014 watu sita wakiwa na pikipiki tatu walivamia kituo kidogo cha Polisi cha Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani na kuua askari mmoja na mgambo wawili, kisha kupora bunduki na risasi 60. 

Julai 12, 2015 kundi la watu kati ya 16 au 18, lilivamia Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga jijini Dar es Salaam na kuua askari wanne na raia watatu kisha yakapora silaha aina ya SMG 15 na simu moja ya upepo. 

Januari 21, 2015 watu waliojihami kwa silaha walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na kuua askari wawili, kisha yakapora silaha zilizokuwapo kituoni hapo.
Silaha hizo zilizoporwa ni aina ya SMG mbili, SAG mbili, Shotgun moja pamoja na silaha mbili za mabomu ya machozi na risasi za SMG. 

Januari 27, 2015 huko mkoani Tanga, watu waliodhaniwa kuwa ni majambazi walivamia na kujeruhi askari wawili waliokuwa doria na kuwanyang’anya silaha mbili aina ya SMG.
Bunduki hizo ni aina ya SMG zenye namba 14301230 na 14303545. 

Februari 3, 2015 kundi la watu lilivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mgeta, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro na kuiba bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30. Pia waliiba jenereta, redio, viti, betri ya gari na spika ya redio.
Machi 30, 2015, askari wawili waliuawa na mmoja kujeruhiwa na majambazi, huko Kongowe jijini Dar es Salaam kisha yakapora bunduki mbili aina ya SMG. 

Mei 29, 2015 watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, walimvamia kwenye lindo askari wa Kikosi cha Tazara jijini Dar es Salaam na kupora bunduki aina ya SMG.
 CHANZO-MTANZANIA

Haya hapa Maajabu Mengine ya Dunia

Kumekua na taarifa nyingi kutoka nchini India kuhusu mtoto wa mwaka mmoja anayeitwa Akash. Taarifa za mtoto huyo zimevuma sana kwa kuwa ana tofauti kubwa na watoto wengine wa mwaka mmoja. Mtoto Akash ameanza kuonyesha dalili zote za kubalehe. Kwa kawaida ulimwenguni kote tunatambua kuwa mwanadamu hubalehe na kuvunja ungo akiwa na umri wa kati ya miaka 10 mpaka 13.mtoto aliyebalehe mapema india
Kwa mujibu wa taarifa hizo mtoto Akash ambaye ana mwaka mmoja anaonyesha mabadiliko yote yanayoonekana kwa mvulana aliyebalehe. Wazazi wake walipompeleka hospitali mtoto huyo alipimwa na kukutwa na kiasi kikubwa cha homoni za kiume kinacholingana na kiasi kile kinachokutwa kwa kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 25. Ingawa habari ya mtoto huyo imevutia watu wengi kwa kuwa ni moja ya matukio yasiyo ya kawaida kuwahi kutokea duniani ninapenda kuchukua fursa hii kukutaarifu kuwa yeye sio mtoto wa kwanza kubalehe mapema na wala hatokua wa mwisho. Hali iliyomtokea mtoto huyu inatambulika kama balehe iliyowahi au kwa kitaalam precocious puberty.
BALEHE ILIYOWAHI (PRECOCIOUS PUBERTY) NI NINI 
balehe iliyotanguliaKi-baiolijia binadamu huzaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzalisha wala kuzaa. Kwa wengi uwezo huo hupatikana wanapofika umri wa miaka kuanzia 10 mpaka 13. Inapotokea binadamu wa kike (msichana) akavunja ungo (kuanza kutoa mayai yaliyo tayari kuchavushwa na kutengeneza mtoto) akiwa na umri wa chini ya miaka nane (8) huwekwa kwenye kundi la waliowahi kuvunja ungo. Inapotokea binadamu wa kiume (mvulana) akabalehe (akaanza kuwa na uwezo wa kutoa mbegu ambazo zinaweza kuchavusha yai la kike na kutengeneza mtoto) kabla ya kufika umri wa miaka tisa (9) nao huwekwa kwenye kundi la waliowahi kubalehe. Balehe iliyowahi au balehe ya mapema au kwa kitaalam precocious puberty ni balehe iliyotokea kabla ya umri wa miaka 8 kwa wasichana na miaka 9 kwa wavulana.
Hali hii si kawaida kutokea na kwa wengi ambao hubalehe mapema huwa wana sababu iliyosababisha wakawahi kubalehe.
BALEHE HUTOKEA VIPI
Mabadiliko ya mwili wakati wa balehe hutokea chini ya muongozo wa ubongo na homoni maalum za jinsia (sex hormones).
mtiririkoBinadamu anapofikisha umri wa kubalehe ubongo hutoa homoni inayoitwa Gonadotropin-releasing Hormone (Gn-RH) ambayo hufanya kazi ya kuamrisha tezi ya Pituitary iliyo kwenye ubongo ili tezi hiyo izalishe homoni za jinsia (sex hormones). Tezi za Pituitary huanza kutoa homoni mbili ambazo ni Luteinizing hormone (LH) na Follicle Stimulating hormone (FSH). Homoni hizo ndio huhusika na uhamasishaji wa uzalishaji wa homoni za kike (Estrogen) kwa wasichana na za kiume (Testosterone) kwa wavulana.
Homoni za kike yaani Estrogen husimamia mabadiliko ya kike kwa wasichana na homoni za kiume Testosterone husimamia mabadiliko ya kiume kwa wavulana.
MABADILIKO YA MWILI WAKATI WA BALEHE
Mabadiliko yafuatayo hutokea wakati wa balehe (kuvunja ungo kwa wasichana)
balehe kwa wote
WAVULANA
Homoni za kiume
  • Mwili kurefuka kwa kasi
  • Sauti kuwa nzito
  • Kuanza kuota ndevu, nywele za kwapani na nywele za sehemu za siri
  • Kukua kwa maumbile ya kiume
  • Kifua kutanuka
  • Kubadilika harufu ya mwili
  • Kutoka chunusi
  • Kupata hamu ya kufanya ngono
Mtoto Akasha ambaye ni mvulana ameonyesha mabadiliko niliyoorodhesha hapo juu akiwa na umri wa mwaka mmoja ndio maana ameushangaza ulimwengu.
WASICHANA (HUVUNJA UNGO)
  • EstrogenKuanza kuona damu ya hedhi
  • Mwili kurefuka kwa kasi
  • Sauti kuwa laini (ya kike)
  • Matiti kuanza kukua kwa kasi
  • Kuota chunusi
  • Kuanza kuota nywele za kwapani na nywele za sehemu za siri
  • Kubadilika harufu ya mwili
  • Kuwa na muonekano wa kike
  • Kupata hamu ya kufanya ngono
NINI HUSABABISHA BALEHE IKATOKEA KABLA YA WAKATI (PRECOCIOUS PUBERTY)
Kwa wengi ambao hali hii hutokea huwa ni vigumu kutambua sababu hasa iliyopelekea wakabalehe mapema lakini kwa ujumla sababu zimewekwa kwenye makundi makubwa mawili.
SABABU ZA KATI (CENTRAL PRECOCIOUS PUBERTY)
mabadiliko ya homoni
mtiririko wa utoaji wa homoni za jinsia
Hizi ni sababu za kwenye ubongo, uti wa mgongo au tezi zinazohusika na uzalishaji wa homoni za jinsia (sex hormone). Sababu hizo ni kama zifuatazo;
  • Uvimbe kwenye ubongo au uti wa mgongo
  • Mapungufu ya kuzaliwa nayo (mfano kichwa kikubwa yaani hydrocephalus)
  • Mtoto kupigwa na mionzi yenye sumu kwenye ubongo au uti wa mgongo
  • Ajali ya ubongo au uti wa mgongo
  • Maradhi ya kurithi ya tezi za adrenal
  • Maradhi ya tezi ya shingo (thyroid gland)
SABABU ZA PEMBENI (PERIPHERAL PRECOCIOUS PUBERTY)
SababuHizi ni sababu zinazohusiana na homoni za jinsia moja kwa moja yaani Estrogen kwa wasichana na Testosterone kwa wavulana.
Kwenye kundi hili la mara nyingi homoni kutoka kwenye ubongo huwa ziko katika kiwango cha kawaida tu. Tatizo hutokea kwenye maeneo homoni za jinsia zinapozalishwa au kutengenezwa.
Tatizo hutokana na hitilafu kwenye tezi za kike (Ovaries kwa wasichana), korodani (kwa wavulana), tezi za Adrenal na tezi za Pituitary.
Sababu huwa ni kama zifuatazo;
  • Uvimbe kwenye tezi za Adrenal au Pituitary ambazo huzalisha homoni za kike (Estrogen) na kiume (Testosterone).
  • Kuongezewa homoni za kiume (Testosterone) au za kike (Estrogen) kutoka nje kupitia vitu kama mafuta ya kupaka au dawa mbali mbali zenye homoni hizi.
  • Kwa wasichana pekee: Uvimbe kwenye tezi ya uzazi (Ovarian tumor)
  • Kwa wavulana: Uvimbe kwenye chembe hai zinazotengeneza mbegu (Germ cells) au kwenye chembe hai zinazotengeza homoni za kiume (Testosterone).
  • Matatizo ya kijenetiki ya kuzaliwa nayo. Haya ni matatizo ya kijenetiki ambayo hutokea wakati wa uumbaji wa mtoto akiwa tumboni kwa mama yake. Matatizo ya namna hii husababisha balehe itokee mapema zaidi kati ya mwaka mmoja (1) mpaka minne (4) baada ya kuzaliwa.
KINA NANI WAKO HATARINI ZAIDI KUBALEHE MAPEMA
  • Wasichana
  • Watoto wenye uzito mkubwa kupindukia
  • Watoto wanaopakwa mafuta yenye homoni za kike au za kiume
  • Watoto wenye maradhi mbali mbali hususani yanayohusu tezi za pituitary, adrenal pamoja na thyroid (tezi ya shingo).
  • Watoto wanaotibiwa saratani kwa njia ya mionzi
MADHARA YA BALEHE YA AINA HII
Watoto ambao wanapitia balehe mapema yaani precocious puberty hupata changamoto mbili kuu
  1. balehe ya mapemaKuwa wafupi wa kimo (kutorefuka sana):Kutokana na kubalehe mapema kabla ya umri sahihi watoto hawa hurefuka wakati huo wa balehe mpaka kufikia kimo kifupi zaidi ya kile cha wale ambao walibalehe muda sahihi wa miaka kuanzia 10. Kutokana na kubalehe akiwa na umri mdogo mhusika hurefuka kwa kasi na baada ya kumaliza kipindi cha balehe uwezekano wa kurefuka kwa kiwango kikubwa hupungua sana kutokana na kukokamaa kwa mifupa.  Watoto wengi wanaobalehe mapema huishia urefu wa chini ya futi 4.
  2. Athari za kisaikolojia: Kutokana na kupitia hali hii kabla ya watoto wengine wa rika lake, watoto wengi hupata athari za kisaikolojia. Athari hizi huweza kuonekana kwa muda mrefu na wengi huhitaji matibabu ya kisaikojolia ili waweze kukubaliana na kilichotokea na kuweza kuishi maisha yao ya kawaida bila kuwaza hali yao yakubalehe mapema.
TATIZO HUGUNDULIKA VIPI
Zaidi ya kuonekana akibadilika na kuonyesha dalili za kubalehe watoto wanaopitia hali hii hutakiwa kupelekwa hospitalini ambako wataonwa na daktari bingwa ambaye atasikiliza historia ya mabadiliko hayo ya mtoto pamoja na kumfanyia vipimo vya kawaida na baadae ataratibu ufanyaji wa vipimo muhimu kuangalia wingi wa homoni za jinsia kwenye miili ya watoto hao.
Kipimo cha wingi wa homoni za jinsia ni kipimo kitakachothibitisha kuwa mabadiliko yanayomtokea mtoto ni balehe.
Pia vipimo vingine vyenye lengo la kugundua sababu hasa ya balehe kutokea mapema ni lazima vifanyike. Vipimo hivi vitasaidia kujua namna ya kukabiliana na mabadiliko yatakayokua yanamtokea mtoto.
MATIBABU
  1. mtoto aliyebalehe mapemaMatibabu yanayolenga kuondoa chanzo cha tatizo: Matibabu haya yanalenga kutibu chanzo cha tatizo (kwa mfano kama chanzo ni uvimbe kwenye tezi za adrenal basi matibabu yatahusisha kuondoa uvimbe huo).
  2. Matibabu ya kupunguza kasi ya mabadiliko ya balehe: Matibabu haya yanalenga kupunguza kasi ya mabadiliko yanayoonekana wakati wa balehe. Matibabu haya huhusisha upunguzaji wa nguvu ya homoni za jinsia.
KUHUSU MTOTO AKASH
Homoni za kiume betterMtoto huyu amefanyiwa vipimo na sababu ya tatizo mpaka sasa haijafahamika hivyo matibabu anayopewa sasa yako kwenye kundi la pili na yanalenga kupunguza nguvu ya homoni za kiume na hivyo kupunguza kasi ya mabadiliko ya mwili yanayotokea kutokana na uwepo homoni hizo (mabadiliko ya wakati wa balehe).


HITIMISHO
Hali hii ya balehe ya mapema hutokea kwa watoto wengi hapa nchini kwetu na ni vyema kama wazazi, walezi wa majirani tujitahidi kuwapunguzia matatizo ya kisaikolojia watoto hawa kwa kukaa nao karibu na kuwahakikishia kuwa hakuna jambo baya ambalo litawatokea. Watakua vizuri tu na wataweza kuendesha maisha yao kama kawaida.
Watoto hawa pia ni vyema itambulike kuwa wanaweza kupata watoto kama ilivyo kwa watu waliopata balehe wakiwa na umri sahihi wa balehe. Hii ina maanisha ni vyema kuwapa elimu ya uzazi na kuhakikisha wanatambua kuwa wao wako tofauti na watoto wengine.
balehe mapema cover
MWISHO
Older Posts
© Copyright CHUNGU CHETU | Designed By CHUNGU CHETU
Back To Top