KAULI za vitisho bado zinaendelea ambapo sasa viongozi wakuu wa jeshi hilo, wanaeleza dhamira ya kutumia nyembo mbalimbali kuhakikisha operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) inazimwa, anaandika Dany Tibason.
Operesheni hiyo ilitangazwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Julai mwaka huu baada ya kufanyika Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi amesema, atatumia kila nyenzo kuzima Ukuta.
Kauli hiyo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari mjini hapa, ikiwa ni siku moja tangu Mbowe, atangaze msimamo wao kwamba, maandamano hayo yatafanyika kama ilivyopangwa.
Amesema, jeshi hilo lina majina ya wanachama wa Chadema wanaopita nyumba kwa
nyumba kuhamasisha watu washiriki maandamano hayo.
Na kwamba, wengine wamejipanga kushambulia polisi hivyo amewataka kutambua kuwa, jeshi hilo lina uchungu wa kuondokewa na askari wenzao walioshambuliwa na baadhi kupoteza maisha hivyo hawako tayari kuendelea kuchezewa.
Hata hivyo, alipotakiwa kutaja majina ya watu hao Mambosasa amesema, yatatajwa baada ya kuwakamata kwasababu, angeyataja wangeweza kutorokea mikoa mingine.
“Serikali siyo polisi pekee, vyombo vya usalama ni pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kata, viongozi wote wa serikali za mitaa, wakaguzi wa
tarafa na polisi kata ambao wanategemewa kukusanya na kutoa taarifa za
kiintelijensia, tutatumia nyenzo zote kuhakikishia wananchi usalama
wao na mali zao,” ameseleza Mambosasa.
Wakati Mambosasa akisema hivyo, Jerad Mambo, Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Dodoma amesema, mikakati yao imekamilika na vijana wana ari ya kutetea haki yao.
Geofrey Mwakiseyo, Katibu wa Chadema wa Jimbo la Mpwapwa amesema, mpaka sasa watu wa kada tofauti katika vitongoji 39 wapo tayari kwa maandamano hayo.
Kuhusu zuio lililotolewa na Kamishna Mambosasa, Mwakiseyo amesema,
anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Nchi kama ambavyo na wao watatekeleza majukumu yao ya kisheria na Katiba hiyo hiyo, kupitia Ukuta.
Kamishna Mambosasa amewataka wanahabari kutohofia usalama wao na kufanya kazi zao hususan kuhusu hali itakavyokuwa siku hiyo ya Septemba Mosi.
Post a Comment