Wanafunzi 316 waliokuwa wakisoma katika Chuo Kikuu cha St Joseph
waliorudishwa nyumbani kwa kukosa sifa, wamefungua kesi ya madai ya Sh6
bilioni kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya chuo hicho
na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Katika kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa Septemba 13 na Jaji
Winfrida Koroso, wanafunzi wanne Ramadhan Kipenya, Innocent Peter, Faith
Kyando na Mohammed Mtunguja waliruhusiwa kuwawakilisha wenzao
mahakamani hapo.
Wanafunzi hao ambao wanatetewa na Wakili, Emmanuel Muga wanaiomba
mahakama iamuru walipwe zaidi ya Sh1 bilioni kama gharama ikiwamo za
ada walizokilipa chuo hicho.
Pia, wanaomba kulipwa Sh5 bilioni kama fidia ya jumla ya gharama za hasara walizozipata.
Wakili Muga ambaye anawawakilisha wanafunzi hao aliiomba Mahakama
kuendesha kesi hiyo kwa haraka, kwa sababu wanafunzi hao wapo mtaani na
hawajui hatima yao huku fedha zao zikiwa zimeliwa.
Chuo Kikuu cha St. Joseph katika kesi hiyo kinawakilishwa na Wakili Jerome Msemwa, huku TCU ikiwakilishwa na Wakili Rose Rutta.chanzo: mwananchi
Post a Comment