Loading...

Breaking News: Rais Magufuli Kiboko ‘awakomoa’ Chadema Arusha

 Mrisho Gambo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha
RAIS John Magufuli amemteua Mrisho Gambo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha (Mjini) kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kumng’oa Felix Kijiko Ntibenda aliyekuwa akishikilia wadhifa huo,anaandika Charles William.
Gambo ambaye kwa muda wa mwezi mmoja sasa, amekuwa katika mgogoro na Godbless Lema, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni kuingiliana majukumu, amepandishwa wadhifa katika mazingira yanayoaminika kuwa, ni ya kimkakati zaidi.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Lema na Gambo walishambuliana vikali mbele ya Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), katika kikao cha pamoja cha watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika kikao hicho, Lema alisema Gambo amekuwa akiingilia uamuzi unaopitishwa na Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo lenye diwani mmoja tu wa CCM kati ya 33.
Huku akitoa mfano kuwa, Kamati ya Mipango Miji ilikuwa imeandaa ziara ya kikazi lakini katika hali ya kushangaza, Gambo alimwagiza Athuman Kihamia, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha aisitishe.
Hata hivyo, Gambo akijibu tuhuma hizo alisema, yeye ndiye rais wa wilaya hiyo kwa sababu anafanya kazi kwa niaba ya Rais Magufuli.
“Mbunge atambue huduma za wananchi hazisubiri maamuzi ya Baraza la Madiwani kwani, haiwezekani kila kamati kutembelea mradi mmoja wa elimu, afya au miradi mingine, Mimi ndiye rais wa wilaya na ninafanya kazi bila kukurupuka,” alisema Gambo.
Katika mvutano huo baina ya Lema na Gambo, Naibu Waziri Jafo alimwagiza Richard Kwitega, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, kutatua mgogoro huo na kuhakikisha kila kiongozi anafanya majukumu yake, pasipo mwingiliano.
Hata hivyo, wawili hao wameendelea kurushiana maneno katika siku za hivi karibuni, Lema amenukuliwa akisema, “Gambo ameingia Arusha na kiherehere huku akikurupuka na kuingilia majukumu yasiyomuhusu.”
Huku Gambo naye akinukuliwa akisema, “Mimi ni mzoefu wa kazi ya ukuu wa wilaya kwa zaidi ya miaka mitano sasa, sihitaji kufundishwa majukumu yangu na mbunge.”
Kupandishwa wadhifa kwa Gambo, kunaashiria kuwa, Ikulu chini ya Rais Magufuli imefurahishwa na kazi yake. Kunaashiria pia katika mgogoro uliokuwa ukiendelea Arusha, Gambo alikuwa akifanya kazi inayokubalika na yenye baraka za Ikulu.
Richard Kwitega, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha ambaye aliagizwa na Jafo kutatua mgogoro wa Gambo na Lema, sasa atakuwa chini ya Gambo. Atakuwa msaidizi wa Mkuu huyo mpya wa Mkoa na atakuwa akifanya kazi kwa maelekezo ya ‘bosi’ huyo.
Itakumbukwa kuwa, katika matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Chadema ilishinda ubunge katika majimbo sita huku CCM ikiambulia jimbo moja tu katika Mkoa wa Arusha na katika Halmashauri ya Jiji hilo, Chadema ilishinda udiwani katika kata 24 na CCM ikiambulia kata moja.
Naam, unaweza kuelezea kitendo cha Gambo kupandishwa wadhifa na Rais Magufuli kwa maneno mengi na kwa namna tofauti tofauti lakini ukisema, “Rais Magufuli amewakomoa Chadema Arusha,” hutakuwa mbali na ukweli.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHUNGU CHETU | Designed By CHUNGU CHETU
Back To Top