BARAZA la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limesema Jeshi la Polisi linawajibu wa kikatiba wa kulinda operesheni yao ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta),anaandika Faki Sosi.
Pastrobas Katambi, Mwenyekiti wa Bavicha, akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, amesema vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa katiba na kwamba vinahaki ya kupatiwa ulinzi vinapofanya mikutano ya hadhara na maandamano.
Katambi amesema jeshi hilo litakuwa linatimiza jukumu lake la kikatiba likishirikiana na Chadema kufanikisha maandamano yaliyopangwa kufanyika nchi nzima Septemba mosi.
Amesema ni upotoshaji mkubwa wa hali halisi pale jeshi la polisi linaposhiriki kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayolenga kuyadhibiti maandamano hayo.
Amesema wapo viongozi wa CCM wenye nia mbaya ambao wanaeneza kampeni kwamba maandamano hayo ni ya uchochezi.
“Sio kweli kuwa Ukuta ni uchochezi na wanaosema hivyo wanalenga kupitisha ajenda yao ya kukichafua chama pamoja na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Chadema,” amesema.
Katambi amesema wakuu wa wilaya na mikoa na wenyewe wanajukumu la kusimamia sheria na katiba ya nchi badala ya kuchukua mkondo wa kutaka kukandamiza demokrasia.
Amesema ni udhaifu tu wa mamlaka ya uteuzi wa viongozi serikalini kuteua makada wa CCM kuwa ndio wanaoshika nyadhifa hizo ambazo huwafanya moja kwa moja kuwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao. Hiyo huwasukuma kutumikia wananchi kwa utashi wa kisiasa kuliko kuzingatia sheria.
Katambi amesema Bavicha limejipanga kuwalinda viongozi wa chama ili wasije kukamatwa kama inavyosemekana polisi kuazimia kufanya hivyo kabla ya siku ya maandamano.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umetangaza kuandaa maandamano nchi nzima tarehe 31 mwezi huu.
Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa umoja huo amewaambia waandishi wa habari leo kwamba maandamano hayo ni ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa alichosema “hatua anazochukua Rais huyo katika kuinua uchumi.”
Shaka amesema wamemuandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu kutaka ruhusa ya kufanya maandamano hayo aliyosema ni ya amani.
Msemaji wa jeshi hilo hakupatikana kuthibitisha kama wamepokea barua hiyo.
Post a Comment