Kwa muda wa miezi kadhaa Lembeli alikuwa kimya, lakini ghafla aliibuka katika mkutano wa Rais John Magufuli na wananchi wa Kahama mkoani Shinyanga na kuanza ‘kujikomba.’“Nipo hapa kwasababu kazi unayoifanya sasa hivi mheshimiwa rais, ndiyo kazi ambayo kwa miaka 10 nikiwa mbunge niliipigania, lakini siwezi kurudi kundini mpaka umesafisha chama kile.”
Hiyo ni kauli ya Lembeli mbele ya Rais Magufuli pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Taifa ambaye alimpa Lembeli nafasi ya kusema jambo kwenye mkutano huo.
Ikiwa ni siku moja tangu Lembeli ambaye alikuwa Mgombea Ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la Kahama, Shinyanga kumshabikia Rais Magufuli, Dk. Makongoro Mahanga amesema, ni upuuzi mtupu.
Dk. Mahanga, aliyekuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na baadaye kujiunga na Chadema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana amesema, hakutarajia Lembeli kutoa kauli tata ya kumshabikia Rais Magufuli.
Kauli hiyo imeonekana kuchefua wengi miongni mwao akiwa Dk. Mahanga ambaye amesema, “rafiki yangu wa siku nyingi Lembeli, kaninyong’onyesha sana, hivi hajui kuwa mazuri yoyote ambayo Magufuli anayafanya, yanafutwa kabisa na utawala wa kidikteta pamoja na uminyaji wa demokrasia?”
Dk. Mahanga amesema, inasikitisha kuona Lembeli akisifia kazi za Rais Magufuli wakati anajua wazi kuwa, miongoni mwa kazi hizo kwa sasa ni pamoja na uminyaji wa demokrasia na vitendo vya kidikteta.
“Lembeli anaposifu kuwa, yanayofanywa na Rais Magufuli hata yeye alikuwa anayapigania miaka 10 iliyopita, ina maana Lembeli alikuwa anapigania nchi hii iendeshwe kibabe, kidikteta na kwa kufinyanga demokrasia?,” amehoji Dk. Mahanga kupitia ukuraa wake wa facebook.
Post a Comment