VIONGOZI na wanachama wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameombwa kujitokeza kwa wingi makao makuu ya jeshi la polisi jijini Dar es Salaam, kufuatilia hatma ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anaandika Mwandishi Wetu.
Lissu Mnadhimu Mkuu wa Upinzani bungeni, aliyekamatwa na jeshi la polisi jimboni kwake Singida Mashariki jana, yuko njiani kuletwa jijini Dar es Salaam kwa mahojiano na jeshi la polisi.
Anatuhumiwa “kumtusi rais wa Jamhuri, John Pombe Magufuli.” Anadaiwa kumuita “dikteta uchwara.”
Kwa mujibu wa ujumbe uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, viongozi wa UKAWA wanaomba kufika kwa wingi makao makuu ya polisi mchana huu kufuatilia hatma ya kiongozi wao.
Akindika katika mtandao wa wabunge wa UKAWA, mbunge huyo machachari wa Ubungo anaeleza, “…kama ilivyoelezwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Tundu Antiphas Lissu, amekamatwa mkoani Singida na sasa yuko njiani kuletwa Dar es Salaam.
Kubenea anasema, kwa kuwa haijafahamika mahali ambako Lissu atafikishwa, anawaomba wabunge wa UKAWA, madiwani, wachama na mashabiki wengine wa vyama hivyo, kujumuika kwa pamoja ili kuungana naye katika dhahama inayomkabili.
Wahe, wabunge, madiwani, wanachama na viongozi wengine wa vyama vinavyounda UKAWA, kwa kuwa hatufahamu Lissu atapelewa katika kituo gani cha polisi, naomba tujumuike kwa pamoja kuelekea makao makuu ya polisi,” anaeleza Kubenea.
Anasema, “huko ndiko tutakaolezwa na mkuu wa jeshi la polisi, IGP Ernest Mangu, mahali aliko Lissu wetu.”
Kubenea amesema, ameweza kuongea na Lissu na kumthibitishia kuwa yuko njiani analetwa jijini Dar es Salaam kutokea Dodoma.
Amesema, katika mazungumzo yake na Lissu, amemueleza kuwa mpaka sasa hajaelezwa na polisi sababu za kumshikilia.
Lissu aliyekamatwa mkoani Singida alilazwa katika kituo kikuu cha polisi cha Dodoma na amesafirishwa alfajiri ya leo kuelekea Dar es Salaam.
Amenyang’anywa simu zake zote mbili kwa madai kuwa amekuwa akifanya mawasiliano na viongozi wenzake, wanachama na familia, jambo ambalo jeshi la polisi limesema, “halikubaliani nalo.”
Mbunge huyo machachari nchini, amekuwa mwiba mkali kwa watawala wa nchi hii; msimamo wake wa kuisema serikali imekuwa ikiwasumbua viongozi wote. Ni msimamo huo ambao umemfanya kusimamishwa na Bunge kwa madai kuwa ameleta vurugu.
Lissu amejitokeza kuwa mmoja wa mashujaa wakubwa aliyejipa jukumu la kukosoa utawala wa Rais Magufuli. Amekuwa akimtuhumu kwa maneno na kalamu kwa kiongozi huyo wa nchi “anaendesha taifa kidekta.”
Kwa mfano, akiandika kuhusu “amri ya Rais Magufuli ya kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye dhahabu nje ya nchi,” Lissu alisema, huo ni ushahidi mwingine, kuthibitisha kuwa Rais haheshimu utawala wa sheria.
Lissu anasema, usafirishaji wa dhahabu nje ya nchi unaofanywa na makampuni ya uchimbaji wa madini yaliyowekeza nchini, umeridhiwa na serikali na unalindwa na mikataba iliyopo.
Kwa mujibu wa sheria ya madini na mikataba ya uendelezaji madini (MDAs), iliyofungwa na Rais Benjamin Mkapa na kurudiwa tena na mrithi wake Jakaya Mrisho Kikwete, mchanga ni mali ya wawekezaji.
Anasema, miongoni mwa makampuni yanayosafirisha mchanga nje ya nchi, ni Mgodi wa Bulyanhulu.
Unayeyusha asimia 70 dhahabu yake nchini na asilimia 30 iliyobaki inafanyikia nchini Japan ambako ndiko kwenye mashine zinazofanya kazi hiyo.
Ndio maana mchanga huo umekuwa unasafirishwa kwenda Japan tangu mwaka 2001.
Hivyo basi, kabla ya rais kutoa “amri yake hiyo,” angeelekeza wawekezaji wajenge kwanza hiyo mitambo yenye uwezo wa kuyeyusha madini ndani ya nchi, kabla ya kupiga marufuku kusafirisha mchanga.
Kwa kuwa wawekezaji hawa wanalindwa kisheria na kimkataba, rais makini alipaswa kushauriana na mamlaka ya madini au kubadili sheria ili upembuzi na uyeyushaji ufanyikie ndani ya nchi.
Badala ya kuwa na rais anayeamini kwamba ametumwa na Mwenyezi Mungu kuinyoosha nchi na neno lake ndio sheria.
Matokeo yake, atagombana na wawekezaji na serikali zao na mabwana wakubwa wa kifedha duniani, ambao ndio wamiliki halisi wa rasilmali zetu.
Watatupeleka kwenye Mahakama za Kimataifa za Migogoro ya Kibiashara ambazo Mkapa na Kikwete walizikubali kuwa ndio mahakama za migogoro kati yetu na hao tuliowapa rasilmali zetu.
Huko hatutapona. Ni kwa sababu tutakuwa tumevunja mikataba na sheria zinazolinda wawekezaji. Muhimu zaidi, hatapata hicho anachokifikiria.
Ni kwa sababu, hatuna uwezo wa ndani wa kuyeyusha madini.
Na, kwa taarifa ya wale wasiojua mambo haya, huo mchanga unaosafirishwa nje sio magwangala. Ni rock waste – mabaki ya mawe – yanayotupwa pembeni ya migodi baada ya dhahabu kutolewa.
Yana madini kiasi kidogo sana ambayo bado yana thamani kibiashara kwa wawekezaji.
Ni makapi yanayoachwa nyuma baada ya karamu ya wawekezaji.
Rais Evo Morales wa Bolivia, alikuwa na mikataba kama hii. Alipochaguliwa Desemba 2006, jambo la kwanza alilofanya ni kuiondoa nchi yake kwenye mahakama za usuhulishi za kimataifa zinazoshughulikia migogoro ya uwezekaji.
Baada ya hapo ndio akabadilisha sheria na mikataba ya uwekezaji iliyoipa Bolivia sehemu kubwa ya umilikaji wa gesi na mafuta ya nchi yake.
Post a Comment