Loading...

YALIYOJILI MUDA HUU: CHADEMA YAJA JUU

 Kamati Kuu ya Chadema wakishikana mikono kuonyesha mshikamano
LICHA ya kuwepo kwa vitisho kutoka mamlaka za juu nchini kuhusu kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimegoma kurudi nyuma, anaandika Dany Tibason.
Kimeeleza kwamba, Operesheni ya Mikutano ya Umoja wa Kuzuia Udikteta nchini (UKUTA) ipo pale pale na kuwa, maandalizi yanaendelea.
Uongozi wa Chadema Kanda ya Kati umeeleza kuwa, maandalizi ya mikutano hiyo yanaendelea na kimewataka wanachama wake kuwa tayari ili kufanikisha mikutano hiyo.
Hivi karibuni Rais John Magufuli alitoa kauli ya kuzuia mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa wabunge ama viongozi mwa chama walio nje ya majimbo husika.
Hatua hiyo imelalamikiwa na kada mbalimbali nchini kwamba, ni uvunjifu wa Katiba ya Tanzania ambayo inatoa uhuru wa kujieleza.
Pamoja na Rais Magufuli kuonya, Chadema kimeeleza kwamba “haki ya mikutano ya kisiasa bila mipaka ndani ya nchi ni ya kikatiba” na kwamba, watafanya mikutano hiyo.
Kauli ya kuwataka wanachama na wenye mapenzi mema na uhuru wa kujieleza nchini kujitokeza kwenye mikutano itakayoanza Septemba Mosi mwaka huu imetolewa leo na Iddi Kizota, Katibu wa Chadema Kanda ya Kati alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Hata hivyo, Kizota amemtaka Rais Magufuli kuacha kuendesha nchi kwa kutoa matamko ambayo yanalivua nguo ama kuliweka njiapanda Jeshi la Polisi.
Amedai kuwa, Rais Magufuli amejikita kwenye matamko na kuipuuza Katiba Nchi jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya taifa iliyojengwa kwa misingi imara na watangulizi wake.
Hata hivyo katibu huyo amesisitiza kwamba, Kanda ya Kati inaendelea na uratibu wa mikutano ambayo itafanyika nchi nzima Septemba Mosi.
“Makatibu wote wa Chadema kwa ngazi zote wanatakiwa kuanza kufanya maandalizi ya mikutano hiyo,” amesema Kizota na kuongeza “Rais anapaswa kuacha kuendesha nchi kwa matamko, afuate Katiba.”
Pia Kizota ameeleza namna chama hicho kinavyokerwa na kamatakamata ya viongozi wa chama hicho inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini.
Amesema, uongozi wa Chadema Kanda ya Kati unaonya tabia ya jeshi hilo kutokana na viongozi hao kukamatwa bila kuwepo kwa sababu za msingi hivyo kusababisha usumbufu sambamba na kurudisha nyuma mikakati ya chama hicho.
“Kwa sasa Jeshi la Polisi limekuwa na tabia ya kuwakamata ovyo viongozi wa Chadema na kuwaweka mahabusu huku wakishindwa kuwapeleka mahakamani kwa wakati.
“Kanda ya Kati inalaani tabia hiyo na hayo yote yanatokana na kutokuwa na kesi ya msingi kwa viongozi hao.
“Kibaya zaidi Jeshi la Polisi limekuwa likivunja sheria kwa kuwanyima dhamana viongozi na wanachama wa Chadema,” amesema Kizota.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHUNGU CHETU | Designed By CHUNGU CHETU
Back To Top