Loading...

Breaking News: MBOWE AMEZUA BALAA ZITO LA KUWATIMUA KAZI VIONGOZI HAWA WAKUBWA NDANI YA CHAMA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema viongozi wa ngazi mbalimbali watakaoshindwa kuandaa maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta), Septemba Mosi, mwaka huu, watakuwa wamepoteza sifa za kuwa viongozi.
 
Mbowe aliyekuwa akizungumza jijini Arusha jana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wakiwamo wabunge na madiwani, alisema watakaoshindwa kuandaa maandamano ya Ukuta ya nchi nzima, watakuwa wamesaliti wananchi ambao waliwachagua.
Chadema imeitisha maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima wiki tatu zijazo, lakini Rais John Magufuli alionya akiwa ziarani Kanda ya Kati hivi karibuni kuwa kutekeleza azma hiyo ni kumjaribu, na "kawaambie... sijaribiwi na sintakaa nijaribiwe."
Lakini akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema kazi ya chama cha siasa ni kuhakikisha serikali inakwenda kwenye mwelekeo sahihi na pale inaposhindwa kufanya hivyo, vyama vya siasa ndiyo kazi yake ya kuipigia kelele, kuinyima usingizi hadi inapokwenda sawa.
“Mkuu wa nchi anataka kuona vyama vya siasa vimelala, sisi hatuvunji sheria, tunafanya haya kwa mujibu wa sheria na tunatambua hakuna mtu yeyote aliyeko juu ya sheria, siyo rais, umoja ama chombo chochote,” alisema Katibu Mkuu wa Chadema.
Alisema chama chake kitaendelea na maandalizi ya kufanikisha operesheni hiyo hadi pale polisi watakaposema kwa sasa nchi inauhitaji Ukuta huo.
“Mpaka sasa tulishavuka kwenye msingi wa ujenzi wa Ukuta, hivi sasa tunakwenda kuuezeka, na huu si wa Chadema, ni wa kila Mtanzania anayeona hakubaliani na kile kinachoendelea katika nchi yake. Kwa hali hii inayoendelea hatuwezi kusema tuache kuujenga,” alisema zaidi.
Mbowe alisema kimsingi kila kiongozi anatakiwa kuelewa kuwa jambo kubwa linalopiganiwa katika Ukuta ni kukandamizwa kwa demokrasia na kukiukwa kwa katiba, masuala ambayo ndiyo yanayowaumiza wananchi waliowaweka madarakani .
"Ni vyema wote mkaelewa kuwa demokrasia ndiyo iliyowaweka madarakani na wananchi wamewachagua ili mwendelee kuitetea kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo lazima tuipiganie kwa nguvu zote," alisema Mbowe.
"Na katika hili, hakuna kurudi nyuma."
Awali, Dk. Mashinji alisema maandalizi katika ngazi ndogo ya kujenga na kuuezeka Ukuta yamefikia pazuri.
Dk. Mashinji alisema kwa namna nchi inavyoendeshwa na kutokana na ombwe la uongozi lililopo, kuna haja ya kuwapo kwa Ukuta huo sasa na si kipindi kingine.
Dk. Mashinji alisema pamoja na vitisho kwa viongozi wake alivyodai vinafanywa na jeshi la polisi katika maeneo mbalimbali, hususani Kanda ya Ziwa, hawatakata tamaa kutekeleza operesheni hiyo.
“Ninavyowaambia hivi sasa Katibu wa chama mkoani Mwanza amekamatwa na wengine bado wanakamatwa kutokana na maandalizi ya operesheni hiyo, lakini tunasema tunaendelea kuweka msingi na Septemba tutaanza kuezeka rasmi,” alisema Dk. Mashinji.
"Tutakutana huko huko na jeshi la polisi, na hapo ndipo tutajua nani anavunja na nani anatekeleza sheria."
Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alikuwa amefuatana na katibu mkuu huyo jana, alisema licha ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu ambako alikiri si kuzuri, yuko tayari kwa ujenzi wa Ukuta.
“Hakuna anayetaka kukamatwa kamatwa, mahabusu si pazuri, lakini tunachotaka kufanya ni kile ambacho katiba inasema," alisema Lissu ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alikamatwa mkoani Singida na kufikishwa Dar es Salaam chini ya ulinzi wa polisi na kufikishwa mahakamani.
"Tuna haki ya kukifanya (maandamano), haki ya kukutana na Watanzania wengine kuzungumza siasa. Tunataka tufanye kile ambacho sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake kinaturuhusu kufanya.
"Mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano halali ya kisiasa kupinga jambo lolote ambalo haliendi sawa.”
Imeandikwa na Elizabeth Zaya, DAR na Asiraj Mvungi, ARUSHA

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright CHUNGU CHETU | Designed By CHUNGU CHETU
Back To Top